Get premium membership and access revision papers, questions with answers as well as video lessons.

Trans-Nzoia District Mock - Kiswahili Paper 2 Question Paper

Trans-Nzoia District Mock - Kiswahili Paper 2 

Course:Secondary Level

Institution: Mock question papers

Exam Year:2006



102/2
KISWAHILI
UFAHAMU ( ALAMA 15)
Soma kifungu kifuatacho halafu ujibu maswali uliyoulizwa
Haki za watoto na wanawake *TRZ*
Makamishina wa Tume za haki za binadamu, waandalizi, waalikwa, watoto, mabibi na mabwana. Kwa muda mrefu kumekuwa na tofauti katika uhusiano baina ya wanajamii. Tofauti hizi zimewapelekea wanawake na watoto kudunishwa. Udunishaji unachukua mwelekeo mbaya zaidi kama watoto ni wa kike.
Kupuuzwa kwa wanawake na watoto kuna historia ndefu. Jambo hili limepata usugu kutokana na
imani hasi zilizoota akilini mwa wanaume na hata wanawake. Rasilimali na majukumu
yamegawanywa kwa misingi inayowatabakisha wanajamii kuanzia wanaume, wanawake halafu chini
kabisa watoto. Katika jamii nyingi, wanawake na watoto wa kike hawarithi chochote ingawa ndio wenye mchango mkubwa katika uzalishaji mali. Aidha mchango wao kuhusu masuala muhimu
nyumbani na katika jamii hupuuzwa hata kama wamesoma kuliko waume na akina baba zao.
Inasikitisha kuwa wanawake na watoto hawana sauti kuhusu uamuzi nyumbani. Wao hulazimishwa
kutenda wanavyoamriwa na wanaume. Kwa mfano, si ajabu mwanamke kulazimishwa kupika pombe
na watoto kusukumizwa kwenda kununua sigara. Yote haya ni kinyume cha matarajio ya Umoja wa
Mataifa kuhusu haki za binadamu.
Ili kuzuia tabia za `ujuaji’, wanaume wengi hupiga marufuku redio, simu, magazeti na televisheni kwa wanawake na watoto. Amri hii hutekelezwa vikali ili wahusika wasijifunze tabia ya kukaidi amri za wazee. Pengine hii ndiyo sababu katika jamii fulani, neno mzee lina maana moja tu; ya wanaume waliokomaa kiumri wala si wanawake. Hii si kweli.
Haki za binadamu ni msingi wa utu. Bila haki hizo mwanadamu hawezi kutumia vipawa na uwezo
wake wa kiakili na kihisia kikamilifu. Udunishaji wa wanawake na watoto unapingana na ukweli huu.
Imani potovu zinazoendeleza uovu huu zimejikita akilini na katika utamaduni. Zinahitaji kuondolewa.
Nafurahi kuwa mmeibua mikakati thabiti ya kulipiga vita tatizo hili. Kwa kweli, sherehe kama hizi ni muhimu sana katika kuwafumbua macho wadau kuhusu haki za wanawake na watoto. Naamini hotuba zilizotolewa hapa zitakuwa mbegu zitakazochipua mabadiliko katika fikra na matendo ya watu.
Yafaa watu wakubali kuwa mke na watoto ni wenza na wadau katika safari ndefu ya maisha.
Nimeona mabango, maigizo, ngoma na michoro ya waume kwa wake, wazee kwa watoto na wavulana
kwa wasichana kuhusu mada hii. Ujumbe umewasilishwa wazi. Ni moyo uliofumwa kwa chuma tu
ambao hauwezi kuathiriwa na ujumbe kuhusu nafasi ya wanawake kurithi na kusikilizwa. Lakini vita vya panga haviamuliwi kwa fimbo. Kilichobaki sasa ni kufanya utafiti wa kukusanya data kuhusu mielekeo na itikadi zinazopingana na lengo letu. Kutokana na matokeo, mikakati iwekwe ili kuvunja nguvu, desturi zinazochochea taasubi za kiume.
Mabibi na mabwana yapasa juhudi zifanywe za kusambaza habari kuhusu umuhimu wa kuheshimu na
kujali binadamu wote na mchango wao. Aidha hatuna budi kuhakikisha nafasi sawa kwa kila mtu
kutoa maoni na kusikizwa. Litakuwa jambo la kusikitisha kama jamii itasahau mchango wa wanawake na watoto katika kuzalisha na kulinda mali. Twahitaji kuondoa uoga kutoka kwa mama zetu wasiotaka mabadiliko. Sekta zote za umma lazima zijitahidi kutekeleza haya.
Ningependa kuwakumbusha kuwa kanuni za ubalozi haziruhusu kuingilia masuala ya ndani ya nchi hii. Hata hivyo, nalazimika kushauri jambo moja. Nashauri ibuniwe wizara ya maendeleo ya wanawake, vijana na watoto. Wizara hii itakuwa na jukumu la kuondoa vikwazo dhidi ya wanyonge.
Kubuni wizara tu hakutasaidia. Wakereketwa washawishi mabadiliko katika sheria kuhusu wanawake na watoto hasa wajane na mayatima. Wanaharakati nao yapasa wahakikishe kuwa sheria hizo zinaheshimiwa. Shirika langu liko tayari kutoa msaada wa kifedha na kitaaluma kwa sababu hii.
Mambo haya yasikomee hapa. Mrudi mlikotoka na mbuni vikundi vya kufuatilia mapendekezo
yaliyotolewa. Ni muhimu kusambaza mliyojifunza hapa ili mambo hayo yapenye kila nyumba katika kila pembe. Kama mlivyoomba, shirika langu litagharamia kuanzishwa kwa mdahilishi katika kila mkoa ili harakati za kupambana na uovu huu katika ulimwengu mzima zifahamike.
Watoto, mabibi na mabwana, nimejifunza mengi kutokana na ari yenu ya kupambana na udhalimu
huu. Nawahimiza mwendeleze juhudi hizo bila kulegeza hata musuli mmoja. Nawatakia ufanisi kwa kila jitihada. Ahsanteni!.
Maswali
1. Kulingana na hotuba hii, ni akina nani wanaobaguliwa zaidi katika jamii? (al I) *TRZ*
2. Ni mambo gani yanayochochea mielekeo mibaya kuhusu haki za kurithi na kusikilizwa katika
jamii? (al 2) *TRZ*
3. Eleza haki wanazonyimwa watoto wa kike katika jamii inayohutubiwa (al 2) *TRZ*
4. Pambanua ushauri aliotoa mgeni kwa ajili ya kutatua udunishaji wa watoto na wanawake
(al 2) *TRZ*
5. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika (al 2) *TRZ*
a) Usugu
b) Rasilimali
6. Eleza maana ya misemo ifuatayo (al 4) *TRZ*
a) Zilizoota akilini
b) Kukaidi amri
c) Moyo uliofumwa kwa chuma
d) Bila kulegeza misuli
7. Methali “vita vya panga haviamuliwi kwa fimbo’’ inatumiwa kumaanisha nini? Eleza
(al 2) *TRZ*
MUHTASARI *TRZ*
Kiswahili, lugha yenye asili yake katika ukanda wa Afrika Mashariki imeenea kote duniani ambako inafundishwa katika vyuo vikuu. Humu nchini, lugha hii inafunzwa katika vyuo vikuu saba vya umma na vyuo vikuu viwili visivyo vya umma. Hivi ni Baratoni na Chuo Kikuu cha Kikatoliki. Katika kiwango hiki, watu wanafunzwa isimu na fasihi. Mafunzo haya yanatolewa kuanzia shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na shahada ya uzamifu.
Elimu ya juu ya kiswahili inatiliwa mkazo katika vyuo vikuu nchini Tanzania na hasa Dar-es-salaamu.
Chuo hiki ndicho mlezi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Kwa muda mrefu, TUKI
imechapisha majarida, kuzua istilahi na kuandaa kamusi. Vyuo vikuu nchini Uganda vikiongozwa na Makerere vimeanzisha mikakati kabambe ya kufunza kiswahili kwingineko barani Afrika, Kiswahili kinafunzwa nchini Msumbiji, Sudan, Misri, Lesotho, Ghana, Nigeria, n.k. Lugha hii imepewa msisimko mkubwa katika mitaa kuambatana na sera ya Afrika Kusini kutukuza lugha za kiafrika.
Ikumbukwe kuwa lugha hii ilichangia pakubwa ukombozi wa Afrika Kusini
Ukitembelea baadhi ya vyuo katika nchi za mashariki ya mbali kama Japani, Korea Kusini, na Uchina,utapata kiswahili kwenye orodha ya masomo. Maandishi mengi yanatafsiriwa kwa kiswahili katika vyuo hivi. Takribani nchi zote Ulaya zina vyuo vikuu vinavyofunza kiswahili. Lakini Uingereza,Ujerumani na nchi za Skandinevia zimetia fora. Pamoja na kufunza lugha hii, vyuo vinafadhili utafiti na uchapishaji wa mambo kuhusu kiswahili. Aidha nchi hizo huwadhamini wengi kusomea huko.
Muhimu zaidi ni kuwa vyuo vikuu katika nchi hizo zimehifadhi maandishi mengi ya kiswahili. Hivi sasa wasomi wengi wanayatumia kufanya utafiti, hasa kuhusu ushairi. Moja ya asasi hizi ni School of Oriental and African Studies, jijini London. Wataalamu waliosomea vyuo hivi wamerudi nyumbani na sasa wanajihusisha na uchapishaji wa vitabu vya nadharia, isimu, fasihi andishi na fasihi simulizi.
Hata hivyo, ni Marekani ambapo matumizi na mafunzo ya Kiswahili katika vyuo vikuu yamepanuka sana. Lugha hii inafunzwa katika majimbo kama Washington, New York, Chicago Texas, California,New Jersey, nk.Vyuo maarufu sana kama vile Cornel, Yale na Havard vinafunza kiswahili. Hali hii imesaidia kuingizwa kwa lugha hii katika mtandao.
Lugha hii inafunzwa kama ishara ya hisia za Uafrika. Wamarekani weusi wanaona fahari kuzungumza kiswahili. Hii huwakumbusha kuwa wao wana asili yao barani Afrika. Kupitia mafunzo haya,
wamarekani wengi wanaiga utamaduni wa Kiafrika. Wengi wao wamejipa majina ya kiswahili kama
vile Baruti, Katembo, Maulana, Simba n,k. Kwa hakika kiswahili kinapata hadhi
Maswali
1. Bila kupoteza maana iliyokusudiwa na mwandishi wa taarifa, fupisha aya ya kwanza na ya pili
(Maneno 50-60) (al 7) *TRZ*
2. Kwa kuzingatia aya zilizobaki, eleza mambo muhimu anayoeleza mwandishi kuhusu
ufundishaji wa kiswahili katika vyuo vikuu (Maneno 60-70) (al 8) *TRZ*
MATUMIZI YA LUGHA
a) Eleza tofauti iliyopo kati ya jozi hii ya sentensi. (al 2) *TRZ*
i) Rehema alinikimbilia
ii) Rehema alinikimbia
b) Yakinisha (hali ya kukubali) huku ukigeuza sentensi ifuatayo katika nafasi ya pili kwa
umoja
(al 2) *TRZ*
Nisiposamehewa na Mola sitapata amani mchana kutwa
c) Eleza matumizi aina mbili ya kiambishi maalum “Ku’’ (al 2) *TRZ*
d) Andika sentensi zifuatazo kwa wingi (al 2) *TRZ*
i) Ngoma ile inalia vibaya kwa kuwa imepasuka
ii) Ni mlango upi uliofungwa na wewe nilipoenda maktabani
e) Tunga sentensi ukitumia vihisishi hivi (al 4)
i) Ahaa!
ii) Taib!
f) Geuza vitenzi vilivyopigiwa mstari viwe majina bila kubadilisha maana ya sentensi
(al 2) *TRZ*
Walimu wanawajibika kuwakomaza vyema wanafunzi wao
g) Andika sentensi zifuatazo kwa kufuata maagizo (al 2) *TRZ*
i) Watoto wanakumbana na dhiki kubwa kuna haki za watoto (Anza: Fauka ya..........)
ii) Tarishi alikula staftahi. Tarishi alienda Ofisini (Anza: Licha ya ...........)
h) Andika neno jingine lenye maana sawa (al 2) *TRZ*
i) Heshima
ii) Ruhusa
i) Eleza maana ya misemo ifuatayo (al 2) *TRZ*
i) Enda jongomeo
ii) Piga unyende
j) Eleza maana mbili ya maneno haya (al 4) *TRZ*
i) Shokoa
ii) Mji
k) Tunga sentensi ukitumia neno “kile’’ kama
a) Kivumishi (al 1) *TRZ*
b) Kiwakilishi (al 1) *TRZ*
l) Eleza tofauti iliyopo kati ya tanakali hizi za sauti (al 2) *TRZ*
Anguka chubwi na anguka tapwi
m) Eleza maana ya methali zifuatazo (al 4) *TRZ*
i) Akumulikaye mchana usiku atakuunguza
ii) Papo kwa papo kamba hukata jiwe
n) Tunga sentensi za kuonyesha kuwa unaelewa tofauti kati ya maneno yafuatayo
i) Gati/ Kati (al 2) *TRZ*
ii) Landa/ Randa (al 2) *TRZ*
o) Andika katika usemi wa taarifa (al2) *TRZ*
“Matokeo mazuri tunayojivunia sasa yamepatikana kwa bidii za wanafunzi na
walimu’’, Mzazi alisema
p) Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya jedwali au mistari/ mishale (al 2) *TRZ*
Askari yule mgeni alimpiga sana mfungwa mgonjwa
ISIMU JAMII
Eleza maana (fafanua) kitanza ndimi kifuatacho kubainisha maana ya panga
i) Ndugu wa kupanga alipanga kwenda kwenye nyumba ya kupanga kumuona ndugu wa
kupanga, akamkuta anapangapanga panga zake, wakapanga kwenda kwenye panga
(al 4) *TRZ*
ii) Eleza madhumuni mawili ya kutunga vitendawili (al 2) *TRZ*
iii) Eleza muundo wa uwasilishaji wa vitendawili (al 2) *TRZ*
iv) Huku ukitoa mifano mwafaka jadili mifano ya aina mbili za nyimbo (al 4) *TRZ*






More Question Papers


Popular Exams


Mid Term Exams

End Term 1 Exams

End Term 3 Exams

Opener Exams

Full Set Exams



Return to Question Papers