Get premium membership and access revision papers, questions with answers as well as video lessons.

Bomet District Mock - Kiswahili Paper 3 Question Paper

Bomet District Mock - Kiswahili Paper 3 

Course:Secondary Level

Institution: Mock question papers

Exam Year:2007



102/3
KISWAHILI
KARATASI YA TATU
FASIHI
JULAI / AGOSTI 2007
MUDA: SAA 2 ½
JARIBIO LA TATHMINI YA PAMOJA WILAYA YA
BOMET 2007
HATI YA KUHITIMU KISOMO CHA SEKONDARI KENYA
(K.C.S.E)
102/3
KISWAHILI
KARATASI YA TATU
FASIHI
JULAI / AGOSTI 2007
MAAGIZO
 Jibu maswali manne pekee.
 Swali la kwanza ni la lazima.
 Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki yaani: Tamthilia,
Riwaya, Hadithi fupi na Fasihi simulizi.
 Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja
Karatasi hii ina kurasa nne zilizopigwa chapa. Mtahiniwa ahakikishe kwamba kurasa zote zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.
1. USHAIRI.
Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yafuatayo
1. Mkata ni mkatika, harithi hatoridhiwa
Sina ninalolishika, wala ninalochukuwa
Mlimwengu kanipoka, hata tone la muruwa!
Mrithi nini wanangu?
2. Sina ngo’mbe sina mbuzi, sina konde sina buwa
Sina hata makaazi, mupasayo kuyajuwa
Sina mazuri makuzi, jinsi nilivyoachwa
Mrithi nini wanangu?
3. Sina kazi sina bazi, ila wingi wa shakawa
Sina chembe ya majazi, mno nikukamuliwa
Nakwa’cheni upagazi, ngumu kwenu ku’tuwa
Mrithi nini wanangu?
4. Sina sikuachi jina, mkata hatasifiwa
Hata nifanye la mana, mno mi kulaumiwa
Poleni wangu sana, sana kwenu cha kutowa
Mrithi nini wanangu?
5. Sina leo sina jana, sina kesho kutwaliwa
Sina zizi sina shina, wala tawi kuchipuwa
Sina wanangu mi sina , sana la kuacha kuraduwa
Mrithi nini wanangu?
6. Sina utu sina haki, mila yangu meuliwa
Nyuma yangu ili dhiki, na mbele imekaliwa
N’nawana na miliki, hadi nitakapofukiwa
Mrithi nini wanangu?
7. Sina ila kesho kwenu, wenyewe kuiongowa
Muwane kwa nyinyi mbinu, mwende pasi kupumuwa
Leo siyo kesho yenu, kama mutajikamuwa
Mrithi nini wananngu?
(a) Taja mambo yoyote mawili ambayo mtunzi angewarithisha wanawe. (alama 2)
(b) Eleza sababu ya mtunzi kutoweza kuwarithisha wanawe.
(alama 3)
(c) Andika ubeti wa nne kwa lugha nathari. (alama 4)
(d) Dondoa mifano miwili miwili ya : (alama 2)
(i) Inkisari
(ii) Tabdila
(e) Chambua shairi hili kwa upande wa :
(i) Dhamira (alama 2)
(ii) Muundo (alama 4)
(f) Eleza maana ya vifungu vifuatavyo kama vilivyotumiwa katika shairi. (alama 3)
(i) Mlimwengu kanipoka
(ii) Sina konde sina buwa.
(iii) Wingi wa shakawa.
TAMTHILIA
Kifo kisimani: Kithaka wa Mberia
2. Eleza mbinu mbalimbali anazotumia Bokono ili kuthibiti na kuendeleza utawala wake katika
Butangi. (alama 20)
3. “Hujambo mtukufu mtemi wa Butangi”
a) Tia dondoo hili katika muktadha wake. (alama 4)
b) Taja na ueleze tamathali ya lugha iliyotumika katika dondoo hili. (alama 2)
c) Eleza sifa anazopagazwa mwenye kuambiwa maneno haya. (alama 10)
d) Ni hali gani inayomfika punde baada ya tokeo hili. (alama 4)
RIWAYA
Mwisho wa kosa : Z. Burhani.
4. Waama, mwisho wa kosa ni vuta ni kuvute ya ukale na usasa.Jadili. (alama 20)
5. Eleza jinsi swala la ndoa lilivyoshughulikiwa katika riwaya ya “Mwisho wa kosa”. (alama 20)
HADITHI FUPI
Mayai waziri wa maradhi na Hadithi nyingine: K.W. Wamitila
Uteuzi wa moyoni:
6. Kwa kurejelea hadithi ya “uteuzi wa moyoni”, onyesha jinsi mwanamke alivyokandamizwa na
jamii. (alama 20)
7. FASIHI SIMULIZI
Soma hadithi hii kasha ujibu maswali
Ilikuwa alfajiri yenye baridi. Umande ulitapakaa kote. Ukungu ulitanda hivi kwamba hungeweza kumwona mtu aliyekuwa hatua chache mbele yako.Ndovu alipoamka, alikuta fisi mlangoni pake. Fisi alikuwa amemlimia ndovu shamba lake, lakini alikuwa hajalipwa ujira wake.
Kila alipomwendea ndovu kwa ajili ya malipo yake, fisi alitiliwa huku na kutolewa kule.”Leo ni leo”,fisi alimwambia ndovu.”Nimevumilia vya kutosha. Kila siku ninapokuja kuchukua pesa zangu, hukosi hadithi mpya ya kunisimulia. Leo sitoki hapa bila pesa zangu!”
Fisi alipomaliza kumwaga joto lake, ndovu alimwambia: “Sikiliza fisi. Mimi nimeheshimika kote kijijini. Naona haja yako ni kunivunjia heshima –mbele ya familia yangu na wanakijiji kwa jumla.
Sikulipi pesa zako, mpaka ujifunze kuwaheshimu wazee. Nakuamuru uondoke hapa mara moja, kabla sijakasirika! Nataka uende popote, unapofikiria kwamba unaweza kupata msaada. Ukienda kwa chifu, usisahau kwamba tunakunywa na yeye. Ukienda polisi, mkuu wa kituo amejaa tele mfukoni mwangu.
Ukienda mahakamani, hakimu tulisoma darasa moja. Popote uendapo, hakuna yeyote
atakayekusikiliza”
“Zaidi ya hayo, hakuna yeyote atakayekuamini.Mimi naitwa Bwana pesa.Kwangu umeota
mpesapesa na kustawi. Nani ataamini kwamba naweza kushindwa kulipa vijisenti vichache
ninavyodaiwa na fisi?”
Fisi alisikiliza kwa makini majitapo ya ndovu. Aliamua kumpasulia ndovu mbarika: “Bwana
ndovu najua kuwa wewe una nguvu na uwezo mkubwa wa kifedha.Lakini hayo yote mimi hayanihusu
ni yako na familia yako. Sitakuruhusu unidhulumu kilicho haki yangu. Usiutumie uwezo uliopewa na Muumba kuwaonea na kuwanyanyasa maskini wasio mbele wala nyuma” alimaliza usemi wake na
kuondoka huku machozi yakimdondoka.
Fisi alipofika nyumbani, aliwasimulia fisi wanyonge wenzake yaliyomsiba.Fisi walikusanyika na kulizingira boma la ndovu huku wakisema: “Tunataka haki itekelezwe! Dhuluma lazima ikome!
Unyanyasaji lazima ukome!” Ndovu aliposikia kelele langoni mwake, alipiga simu kwenye kituo cha polisi.
Mara, kikosi cha polisi wa kupambana na ghasia kiliwasili. Fisi walipigwa mijeledi na kuezekwa marungu. Waliojifanya mabingwa walipigwa risasi. Fisi waliosalia walikimbilia makwao, huku
wakichechemea kwa maumivu. Mpaka wa leo fisi wangali wanatembea kwa kuchechemea.
Maswali
(a) Usimulizi huu ni wa aina gani? Toa sababu. (alama 4)
(b) Eleza tamathali za usemi zilizotumika katika hadithi hii. (alama 4)
(c) Eleza sifa za ndovu katika hadith hii. (alama 5)
(d) Fafanua jinsi kisa hiki kinavyo dhihirisha methali: ‘Mwenye nguvu mpishe’ (alama 4)
(e) Je, hadithi zina umuhimu gani katika jamii? (alama 3)






More Question Papers


Popular Exams


Mid Term Exams

End Term 1 Exams

End Term 3 Exams

Opener Exams

Full Set Exams



Return to Question Papers