Get premium membership and access questions with answers, video lessons as well as revision papers.

Alifa chokocho na Dumu Kayanda: Tumbo Lisiloshiba 'Doa ndio kawaida inayobainisha maisha ya mwanadamu.'Onyesha ukweli wa kauli hii kwa mujibu wa hadithi za: Shogake Dada ana...

      

Alifa chokocho na Dumu Kayanda: Tumbo Lisiloshiba

'Doa ndio kawaida inayobainisha maisha ya mwanadamu.'Onyesha ukweli wa kauli hii kwa mujibu wa hadithi za: Shogake Dada ana Ndevu, Mame Bakari, Shibe Inatumaliza na Mtihani wa Maisha.

  

Answers


Martin
Swali hili linatahini uozo. Doa iangaliwe kama mapungufu ya tabia ila si hali (umaskini)

Shogake Dada ana Ndevu

(i) Mkadi anasemwa kuwa mwenye sura nzuri ila ana mienendo mbi. Bi. Hamida anaeleza kuwa tabia zake mbaya afadhali zile za mbwa koko ithibati ya kuwa hakuwa mwadilifu (Uk 29)
(ii) Safia anawahadaa wazazi wake kuwa Kimwana ni shoga yake ambaye walisaidiana kudurusu masomo. Ukweli ni kuwa Kimwana ni mpenzi wake ( Uk 30)
(iii) Kimwana anajibeba kwa heshima kuu hata wazazi wake Safia wakaishia kumwamini. Anajitanda buibui na hasemi nao. Hivi hawapati kutambua kuwa ni mwanaume ambaye alijitia kuwa mwanamke ili apate fursa ya kutoshelezana kimahaba na Safia. (Uk 31)
(iv) Kimwana na Safia wanajitia kujifungia chumbani “kusoma pasi na usumbufu”. Baadaye inabainika kuwa kubukua huku walikozamia kulikuwa ni kutoshelezana kimwili ( Uk 32)
(v) Ujasiri wa Safia na Kimwana kurushana roho wazazi wake Safia wakiwa sebuleni ni uozo usio kifani. Haiwapigi mshipa kwamba wapo pale nyumbani watu wazima ambao wasingekubaliana na kitendo kile kuendelea. Wanawakosea heshima kwa kushiriki ya faraghani wakifahamu fika kuwa walikuwepo mahali pale (vi) Safia anapopambazukiwa kuwa amehimili, anasingizia ugonjwa. Mamaye amsailipo kuhusu kubadilika kwa hali zake anasisitiza kuwa alikuwa kapimwa zahanatini na kubainika kuwa mgonjwa wa malaria sugu; hasemi ukweli.(Uk 33)
(vii) Safia anawazia kuavya mimba aliyokuwa ameihimili. Anakufa katika harakati za “kufanikisha” njama hii mbaya. (Uk 35)
(viii) Bwana Masudi na Bi. Hamida wanaonyesha uozo mkubwa. Wanafanya kikao cha kuwasema watoto wa wenzao. Kwa mfano, wanamwumbua Mkadi kwa matendo yake. (uk 29)
(ix) Bwana Masudi na Bi. Hamida wanayatelekeza majukumu yao ya uzazi. Hawa wanashawishika kirahisi kuwa Kimwana ni shogaye Safia. Hawafanyi jitihada zozote kumjua wala kufahamu ikiwa kwa kweli wawili hawa walikuwa wakijifungia kusoma kama walivyosingizia. Hatimaye Safia anakuwa mja mzito.
(x) Ni dhahiri kuwa katika jamii hii wapo wahudumu wa sekta ya afya ambao wako radhi kuwasaidia wasichana wanaotaka kuavya mimba kutekeleza kitendo hicho haramu. Safia anakufa akisaidiwa kuavya mimba pale katika kliniki. (uk 35)

Shibe inatumaliza:

(i) Mzee Mambo anashikilia wadhifa wa waziri kivuli ila anakiri kuwa hana kazi maalum. Anapata mshahara kwa kutofanya lolote. Anakiri kwamba hana kazi hata moja tu Huku ni kuuibia umma na serikali. (uk 36-37)
(ii) Serikali inaendeleza ubadhirifu. Mzee Mambo anakiri kuwa na vyeo viwili na hana kazi yoyote ile aifanyayo. Hata katika wizara ambapo yeye ni waziri wa kivuli yupo waziri anaye fahamika. (uk 37). Licha ya kufahmu hivi serikali inampa nyadhifa anazozishikilia tu.
(iii) Mzee Mambo amejawa unafiki. Licha ya kuwa ni bayana hata kwake kuwa anafaidi pasipofaa anaeleza jinsi wakati mwengine yeye hujivika uchamungu na kujiliwaza kwa maandishi matakatifu. (uk 37).
(iv) Mzee Mambo anaongozwa na tamaa na ubinafsi. Anakiri kuwa vyeo vyake vinampa fursa ya kupakua mshahara. Anajinaki kuwa yeye si wa kupewa mshahara bali wa kujipakulia, kupapia na kufakamia. Huu ni uroho na ubinafsi wa hali ya juu. (uk 37)
(v) Mzee Mambo anatumia raslimali za umma visivyo. Sherehe za kuadhimisha mwanawe mmoja kuota meno na mwenziwe kuingia nasari zinapeperushwa moja kwa moja na runinga ya taifa. Magari kutoka ikuluni yanasafirisha, chakula,jamaa zake,mapambo na hata maji kwa sherehe hii. (uk 38-39)
(vi) Sasa na Mbura pia wanakiri kuwa wanafanya mengi katika wizara ya mipango na mipangilio ila hawana lolote la mno wanalolifanya. (uk 38). Usemi huu unaonyesha watu wasiofahamu majukumu yao wala kuyachukulia kwa umuhimu unaofaa.
(vii) Tamashani, Sasa na Mbura sawa na wageni wengine wote wanakula kilafi. Wanaonekana kurudi awamu kadha kujitilia chakula tena chenyewe shinda! Maelezo haya yanatuonyesha watu waliotawaliwa na uroho mno. (uk 41).(viii) D.J na wenzake serikalini wanaelezwa kuchota mabilioni ya fedha kwa sherehe inayoandaliwa na Mzee Mambo. (uk 42). Huu ni ufisadi mkuu.
(ix) Pia, D.J huyu anamiliki duka kubwa la dawa ambalo linasambaziwa dawa zenyewe kutoka bohari kuu ya dawa za serikali. Kwa jinsi hii analiibia taifa na haswa wagonjwa ambao wanazitegemea dawa zile kupata nafuu. ( uk 43)
(x) D.J anaelezwa kupata huduma za kimsingi bila ya kuzilipia ilhali wananchi wengine wa kawaida wanazilipia licha ya ufukara wao. (uk 43) Hali hii inabainisha ubinafsi na ufisadi uliomtawala pamoja na waliotwika jukumu la kuhakikisha kuwa huduma hizi zimewafikia wote.
(xi) Mbura anaangazia uroho uliowatawala waja. Anasema kuwa waja walikula vyao na vya wenzao. (uk 44). Kauli hii inaashiria kutoridhika na yale ambayo mja amejaliwa. Uroho wao unawatuma kula hata vya vizazi ambavyo havijazaliwa.
(xii) Ubaguzi wa kitabaka umebainika. Mbura anazidi kusaili sababu ya walio mamlakani au karibu nayo kuzidi kula kwa niaba ya wenzao. (uk 44). Anasikitika kuwa wao wanazidi kuyajaza matumbo yao ilhali wananchi wa kawaida wanazidi kudhikika.
(xiii) Watu wametawaliwa na ukatili. Mbura anaeleza kuwa watu wanauana kwa mabomu, risasi na kunyongana kwa sababu ya kutafuta faida za kibinafsi. (uk 44)
(xiv) La kusikitisha ni kwamba ingawa waja wanafahamu kuwa wanatenda yasiyofaa, hawaonekani kujali lawama. Wamehalalisha haramu na kuyafanya matendo hayo ya kawaida mno. (uk 44)

Mame Bakari:

(i) Sara anabakwa na janadume moja katili. Janadume hili linaongozwa na uchu wa kujitosheleza kimwili kumhujumu Sara vibaya hivyo. (uk 47)
(ii) Janadume linalombaka Sara lianaelezwa kuwa na haraufu kali ya kutuzi. Hili halijali mambo ya kimsingi kama usafi wa mwili. (uk 47)
(iii) Jamii inaonyeshwa kuwa isiyowahurumia wasichana wanaobeba mimba ama kwa kubakwa ua kwa kushiriki mahaba kwa hiari yao. Sara anawazia kutengwa na kukashifiwa na jamii yake pindi watakapogundua uja uzito wake. (uk 48)
(iv) Babaye Sara anaonyeshwa kuwa katili/ mkosa utu. Sara anaeleza sababu za kutomjuza kuwa alikuwa amebakwa. Anasema kuwa babaye alikuwa mkaidi ambaye alikuwa na tabia ya kutoamini maafa ya mwengine. (uk 48)
(v) Wanaume wanaonyeshwa kuwa wasio utu. Inabainika kuwa hata mwanamke anapobakwa mwanaume halaumiwi bali ni mwanamke aliyehasiriwa. (uk 48)
(vi) Usaliti umebainishwa. Sara anawazia jinsi wengi wa jamaa zake, majirani na wanafunzi wenziwe wangetengana naye pindi uja uzito wake ungebainika. (uk 49)
(vii) Uavyaji wa mimba umebainishwa. Kwa kipindi kifupi Sara anawazia kuitungua ile mimba aliyoihimili ila anajirudi. Mawazo haya ya kutungu amimba ni ishara tosha kuwa shughuli hiyo ipo na inaendelezwa katika jamii yake. (uk 50)
(viii) Umma unaolifumania janadume lililombaka Sara katika kisa tofauti cha ubakaji, unalipiga kipopo. Ingawa kitendo chake cha ubakaji ni cha kikatili, ni ukatili mkubwa kumpiga hata kumwua badala ya kumfikisha kituoni kufunguliwa mshtaka.

Mtihani Wa Maisha:

(i) Ufidhuli wa waja umebainishwa. Samueli aingiapo afisini kuyapokea matokeo yake anakumbana na mwalimu mkuu ambaye katika mawazo yake anamweleza kuwa hambe ambaye hakuwahi kumwamini. (uk 132). Huu ni ukosefu mkuu wa heshima.
(ii) Mwalimu Mkuu anadhihirisha dharau kwa namna anavyoingiliana Samueli. Anamtupia bahasha yenye matokeo yake, kitendo kinachodhihirisha jinsi alivyomdunisha Samueli. (uk 133)
(iii) Babaye Samueli ni mwenye taasubi ya kiume. Aliwaona binti zake kuwa wanawake tu. Ingawa walikuwa wamefikia ufanisi mkubwa nasomoni hakuwathamini kama alivyomthamini Samueli. (uk 136) Fahari yake ilikuwa kumwona Samueli akifaulu.
(iv) Wanafunzi wanashiriki mahusiano ya kimapenzi wangali wachanga. Samueli anahusiana kimapenzi na Nina ingawa wote ni wanafunzi wa umri mdogo. (uk137)
(v) Samueli anawadanganya wazazi wake kuwa hakupewa matokeo yake kwa kuwa hakuwa amekamilisha kulipia karo yake. Ukweli ni kuwa alikuwa amefeli mtihani na Licha ya kuyajua hayo na kuwa nayo, hakuwataka hawa kuyatambua. 9Uk 137)
(vi) Ukatili pia umejitokeza katika kazi hii. Babaye Samueli anafika kidimbwini ambako |Samueli alikuwa anajaribu kujitoa uhai akiwa amebeba kamba aliyokusudia kumpa ajinyongee na kufilia mbali. Hamwonei huruma katika hali zile za utamaushi. (uk 139).

Tanbihi:

(i) Ni sharti mwanafunzi aangazie hadithi zote nne.
(ii) Kila hadithi ina mifano tosha ya uozo kwa hivyo mwanafunzi aaangazie mifano mitano mitano ya uozo kutoka kwa kila hadithi.
Swali hili ni wazi kwa hivyo mwanafunzi asihiniwe kwa kupendekeza hoja za ziada. Mradi ana hoja atuzwe kwa hoja zozote tano kwa kila hadithi.
(iii) Baada ya kupata hoja tano, nyingine zichukuliwe kuwa za ziada.

marto answered the question on September 24, 2019 at 07:51


Next: Simplify;
Previous: The figure below shows the graph of Log P against Log Q. Given that P = aQn , find the value of a and n

View More Kiswahili Fasihi Questions and Answers | Return to Questions Index


Learn High School English on YouTube

Related Questions