Matumizi ya sheng' yameshamiri sana nchini Kenya hasa miongoni mwa vijana.(Solved)
Soma taarifa inayofuata kisha uyajibu maswali
Matumizi ya sheng' yameshamiri sana nchini Kenya hata miongoni mwa vijana. Ni kilugha ambacho kinakisiwa kuzuka katika miaka ya 60 na 70 katika makazi ya mashariki mwa jiji la Nairobi kama vile Kaloleni, Mbotela/ Bahati na kadhalika.Kwa sasa ni kilugha kilichoenea kwingi nchini Kenya na kuwa kitambulisho cha takriban vijana wengi. Wataalam mbalimbali wanabainisha nadharia mbalimbali kuhusu chanzo cha lugha hii. Kuna nadharia mbili kuu kuhusu asili ya lugha ya Sheng: kwamba kilugha hiki kiliibuka kutokana na wahuni na wakora jijini Nairobi ambao lengo lao Iilikuwa kuwasiliana kwa siri. Nadharia nyingine ni kuwa kilichipuka kutokana na vijana ambao walizua lugha ya kuwasiliana baada ya uhuru (kwa sababu walikichukia Kiswahili ambacho walikiona kama lugha ya uboi)
Dhana hizi kwa muda mrefu, zimeathiri mitazamo kuhusiana na kilugha hiki. Kwa sasa ni kilugha ambacho ,yjiasambaa katika sehemu mbalimbali za Kenya na watu wa matabaka mbalimbali wanakitumia. Kilugha hiki kimeanza kuashiria uhalisia mkubwa wa maisha ya kisasa, zaidi katika jamii ya Wakenya. Aidha, sheng imejitanzua kutoka hali ya kuwa kilugha cha maongezi pekee na sasa kinatumiwa katika baadhi ya vitabu, hata waandishi wa vitabu wameanza kukitumia. Kwa mfano, katika miaka ya 80, David Mailu katika kitabu chake 'Without Kiinua Mgongo' alitumia Sheng. Katika siku za hivi karibuni, riwaya ya 'Kidagaa Kimemwozea' iliyoandikwa na Ken Walibora kilugha cha sheng kimepewa nafasi kama kitambulisho cha vijana kupitia kwa mhusika DJ Bob.
Vilevile kumezuka vyombo vya habari kama redio, mfano idhaa ya Ghetto, redio ambayo inaendeleza mawasiliano kwa matumizi ya Sheng. Kuna vipindi vya matangazo ya kibiashara katika runinga ambayo yanaendelezwa kwa Sheng. Kwa mfano, katika 'gazeti la Taifa Leo, kuna ukumbi wa 'Mchongoano' ambao umekuwa ukiendelezwa kwa Sheng.
Nchini Kenya ambapo asilimia 60% ya idadi ni vijana, Sheng imetokea kuwatambulisha vijana. Katika enzi hii ya Teknohama. wanaomiliki vyombo vya habari na sekta nyingine za biashara wamegundua kuwa matumizi ya Sheng ndiyo njia mwafaka zaidi ya kulifikia soko kubwa la vijana kwa ajili ya kueneza matangazo ya bidhaa na huduma za kibiashara. Kwa hivyo, Sheng imekuwa daraja la kuwafikia na kuwavutia vijana.
Hata hivyo, kwa upande mwingine matumizi ya Sheng yamelaumiwa na walimu wengi katika shule za msingi na zile za upili kuwa ni sababu mojawapo kuu ya kushuka kwa matokeo ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza miongoni mwa wanafunzi. Sheng imelaumiwa kwamba inasababisha wanafunzi kutozingatia mafunzo ya kanuni za sarufi na tahajia au maendelezo. Wataalam wanadai kuwa ni msimbo ambao hauzingatii sheria za sarufi na tahajia kwa sababu zisizofahamika, kwani ingawa muundo wake wa kisarufi hushahabiana na ule wa Kiswahili, Sheng hupuuza sarufi ya Kiswahili katika matumizi yake.
Ingawa sheng imekuwa ikipigwa vita, kuna wataalam ambao wana mtazamo kwamba juhudi hizo haziwezi kufanikiwa kwani Sheng ni chombo cha mawasiliano miongoni mwa vijana na kwa hivyo ina umuhimu wake ambao hauwezi kufumbiwa macho. Wanasema kuwa ni chombo ambacho kinafumbata hisia na mshikamano wa kizazi kipya kama ilivyojitokeza katika kauli mbiu ya mgombeaji urais mwaka wa 2012,'Tunawesmake.
Katika hali ambapo kiwango cha ubora wa matokeo ya Kiswahili yalidorora katika mtihani wa kidato cha nne (KCSE) mwaka wa 2012 na kuwa asilimia 35.81 pekee yakilinganishwa na asilimia 48.82 ya mwaka 2011, Sheng imekuwa ikilaumiwa kuwa ndicho chanzo cha kudorora kwa viwango vya ubora wa matokeo. Baadhi ya hao wataalamu wanasema kwamba Sheng haipaswi kuhujumiwa. kinachohitajika kufanywa ni kuwaelimisha vijana kuhusu mipaka ya matumizi yake.
Maswali
a) Taja mada ya kifungu hiki.
b) Fafanua nadharia mbili zilizoeleza asili ya lugha ya sheng.
c) Eleza matumizi bainifu ya kilugha cha Sheng katika jamii ya sasa.
d) Taja matokeo hasi ya matumizi ya Sheng katika jamii.
e) Ni kwa nini mwandishi Walibora ameshirikisha matumizi ya Sheng katika kazi yake ya Kidagaa Kimemwozea
f) Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika kifungu hiki.
i) Teknohama
ii) kudorora
iii) msimbo
iv) Kuhujumiwa
Date posted: September 25, 2019. Answers (1)
"Ingawa walifahamu sababu ya kuitwa pale mpango uliokuwepo ulikuwa usiku wa giza."(Solved)
Damu Nyeusi na Hadithi nyingine : Ken Walibora na Said A. Mohamed
"Ingawa walifahamu sababu ya kuitwa pale mpango uliokuwepo ulikuwa usiku wa giza."
(a) Fafanua muktadha wa maneno haya.
(b) Eleza tamathali iliyotumika katika dondoo hili.
(c) Onyesha vile wahusika mbalimbali hadithini waiivyoathiriwa na sababu ya kuitwa pale.
Date posted: September 25, 2019. Answers (1)
RIWAYA YA KIDAGAA KIMEMWOZEA.
Mtoto ni mtoto hata likiwa bonge la nyama. Mtu hupata ajaliwalo sio alitakalo.
(Solved)
RIWAYA YA KIDAGAA KIMEMWOZEA.
Mtoto ni mtoto hata likiwa bonge la nyama. Mtu hupata ajaliwalo sio alitakalo.
(a) Fafanua muktadha wa dondoo hili.
(b) Eleza tamathali ya lugha iliyotumika katika usemi huu.
(c) Ukirejelea riwaya thibitisha kuwa mtu hupata ajaliwalo silo alitakalo.
Date posted: September 25, 2019. Answers (1)
Mbona isiwe kweli? Wewe panga uwalete tule matunda ya jasho letu nao watoto.(Kwa kurejelea tamthilia "Mstahiki Meya")(Solved)
Mbona isiwe kweli? Wewe panga uwalete tule matunda ya jasho letu nao watoto.(Kwa kurejelea tamthilia "Mstahiki Meya")
(a) Eleza muktadha wa dondoo hili.
(b) Eleza mbinu mbili za uandishi katika dondoo hili.
(c) Eleza yaliyopangwa baada ya usemi huu.
Date posted: September 25, 2019. Answers (1)
Ole wangu! Ole wangu, nisikize Mola wangu,(Solved)
Ole wangu! Ole wangu, nisikize Mola wangu,
Lipokee ombi langu, wanisikize wenzangu,
Washike ujumbe wangu, uloleta Mola kwangu,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Amri kumi za Mola, mumekwisha zikiuka
Ndipo hamuwezi lala, mumekwisha vurugika,
Mumemsahau Mola, ndipo nanyi mwasumbuka,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Mwaabudu mashetani, ushirikina ni mwingi,
Munaiba hadharani, waongo nao ni wengi,
Mwajawa na taraghani, na wazimu mwingi,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora,
Mwauana ovyoovyo, mwasemana ndivyo sivyo,
Fitina nazo zilivyo, mwarogana vivyo hivyo,
Matusi ni vile sivyo, munaisha ka isivyo,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Kuna dawa za kulevya, na hata pembe haramu,
Na ukimwi nakujuvya, unaua wanadamu,
Na mimba nazo kuavya, watoto ni marehemu,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Wengine nao hudai, waoe jinisi moja,
Ati mwingine hafai, heri sawia ya mja,
Haya maoni ni hoi, tupinge kila mmoja,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Ploti mwazinyakua, na viwanja vya mipira,
Makaburi mwala pia, mabibi mwateka nyara,
Ibada zikifikia, mwafurika kwa majira
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Wengi tuwachaguao, si viongozi ni waizi,
Tamaa walio nao, yaongoza maamuzi,
Mishahara ile yao, huongezwa kila mwezi,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Usalama hatunao, wasiwasi umezidi,
Waja kiwa makazio, huogopa magaidi,
Mabomu walipuao, huruma wamekaidi,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
Beti kumi namaliza, dua yangu imetimu,
Mungu amekwisha anza, kuhukumu mwanadamu,
Wote walojipotoza.waiepuke hukumu,
Nyakati tunazoishi, ni Sodoma na Gomora.
MASWALI
(a) Lipe shairi hili kichwa mwafaka.
(b) Shairi hili linaweza kuwekwa katika bahari kadhaa. Taja na ueleze bahari zozote tatu.
(c) Taja na ueleze mbinu tatu za lugha zilizotumiwa katika ubeti wa kwanza.
(d) Eleza sababu ya mshairi kutumia alama ya ritifaa katika ubeti wa nne
(e) Tambua uhuru wa kishairi uliotumika katika ubeti wa tisa mshororo wa tatu na ueleze umuhimu wake.
(f) Andika ubeti wa sita kwa lugha tutumbi.
(g) Taja mifano mitatu ya uozo anaolalamikia mwandishi.
(h) Eleza toni ya mwandishi.
Date posted: September 25, 2019. Answers (1)