Zaraa ndio uti wa mgongo wa taifa la Kenya. Viwanda vingi nchini hutegemea kilimo kama malighafi yake na kuwalisha wafanyakazi

      

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
Zaraa ndio uti wa mgongo wa taifa la Kenya. Viwanda vingi nchini hutegemea kilimo kama malighafi yake na kuwalisha wafanyakazi. Licha ya umuhimu wa sekta hii, mkulima ambaye ndiye nguzo za zaraa anaendelea kukabiliwa na matatizo mbalimbali yanavokwamiza juhudi zake.
Mojawapo ya matatizo yanayomkabili mkulima ni ukosefu wa ushauri wa zaraa. Wataalamu wanaotarajiwa kumshauri mkulima kuhusu njia bora za kuzalisha na kuongeza pato lake ni haba ikilinganishwa na idadi ya wakulima wanaohitaji ushauri. Wachache walioko nao wanakwamizwa na mambo tofauti. Mathalani, utawapata hawaendi nyanjani ili kukutana na wakulima kwa kuwa hawana usafiri. Iwapo usafiri upo, huenda petroli ikawa ni kizungumkuti. Halikadhalika, usisahau kuwa baadhi ya wataalamu hawa ni walazadamu au mafisadi. Kuna wale wanaofika ofisini na kushinda siku nzima wakisoma gazeti huku wakijaza miraba, wakicheza bao au karata. Kuna wale nao ambao hufika ofisini wakaangika koti au sweta kitini ili waonekane kuwa bado wapo na kisha kutokomea kwenda kushughulikia mambo yao ya kibinafsi yasiyohusu ndewe wala sikio kazi waliyoajiriwa kuifanya.
Ukosefu wa sera mwafaka kuhusu ardhi nalo ni tatizo jingine linalotatiza kilimo nchini. Serikali haijaweka sera mahususi kuhusu matumizi ya ardhi. Wananchi wengi huongozwa na taratibu za utamaduni wa nasaba zao. Taratibu hizi hupendekeza ugawaji wa ardhi kwa minajili ya urithi kulingana na warithi waliopo. Si ajabu kuwa kote nchini, ardhi inayofaa kwa kilimo imekatwakatwa vipande vidogo vidogo ambavyo haviwezi kuwa na faida kwa zaraa.
Kushindwa kwa mkulima kuongeza virutubishi ardhini ni changamoto nyingine inayokabili kilimo nchini. Ulimaji wa kile kipande cha ardhi mwaka nenda mwaka rudi, bila kukipa nafasi ya kukipumzisha, huufanya mchanga kupoteza virutubishi muhimu vinavyohitajiwa na mimea. Hili nalo huchangia kupunguza uzalishaji wa mazao. Ili kutatua tatizo hili, wakulima wengi hukimbilia mbolea za kisasa ambazo badala ya kumsaidia, humwongezea madhila. Mbolea hizi zinatambulikana kuchangia uchafuzi wa mchanga na ardhi.
Mabadiliko ya hali ya anga nayo huongeza msururu wa madhila ya mkulima. Mabadiliko haya yamemfanya mkulima kushindwa kupanga wakati anaotakiwa kutayarisha shamba, kupanda, kupalilia, kunyunyizia dawa na kadhalika. Mvua imekuwa adimu. Badala yake panakuwa na vipindi virefu vya kiangazi ambavyo huathiri bidii za mkulima. Maji nayo yanaendelea kupungua na wakulima wengi hawawezi kukimu mahitaji ya unyunyizaji maji mashambani.

(a) Andika anwani inayofaa kifungu hiki.
(b) Huku ukirejelea kifungu, fafanua umuhimu wa kilimo hapa nchini.
(c) Eleza changamoto tatu zinazowakabili wataalamu wa kilimo
(d) Mbali na matatizo yanayowakumba wataalamu onyesha matatizo mengine matatu yanayokumba sekta ya zaraa. (alama 6)
(e) Eleza maana za msamiati ufuatao kulingana na taarifa.
(i) yanayokwamiza
(ii) sera
(iii) adimu

  

Answers


sharon
(a) Zaraa / Kilimo
(b) i) Ni uti wa mgongo wa taifa
ii) Viwanda vingi hutegemea malighafi yake.
iii) Huwalisha wafanyakazi, zozote
c) i) Ni wachache ikilinganishwa na wakulima wanaohitaji msaada wao.
ii) Hawana usafiri
iii) Petroli ni kizungumkuti
d) Ukosefu wa sera mwafaka kuhusu ardhi.
- Wananchi wengi huongozwa na taratibu za tamaduni za nasaba zao.
- Kushindwa kwa mkulima kuongeza virutubishi ardhini.
- Mbolea huchangia uchafuzi wa mchanga.
- Mabadiliko ya hali ya anga. za kwanza
e) Yanayotatiza.
- Mpangilio / utaratibu / rnikakati.
- Haba / nadra.
sharon kalunda answered the question on October 3, 2019 at 07:56


Next: Outline the different types and forms of instructional media.
Previous: List the steps involved in historical research

View More Kiswahili Questions and Answers | Return to Questions Index


Exams With Marking Schemes

Related Questions