i. Starehe na Anasa.
Emmi anashangazwa na tabia ya Tembo ya kujistarehesha kwa anasa za pombe. Anamkumbusha kuwa anasa za dunia hii hawezi kuzimaliza. Anajitia bingwa wa dunia na kusahau alikotoka, hali ambayo inamletea madhara na kumlaza hospitalini.
Siku ya kisanga kikuu, Tembo anaamshwa na mkewe kunywa staftahi. Anapomalizia saa sita, anamhepa mkewe na kuelekea kujistarehesha mtindini. Anawapata wenzake huko na wanakunywa kwa kikoa. Kila mmoja ana zamu ya kununua pombe.
Hata baada ya kituko cha Moshi, bado Tembo na wenzake wanaelekea kuzima kiu kwingine. Wanakunywa pombe ya kima cha chini wanayoweza kununua. Baadaye wanaingia jukwaani kusakata densi.
Tamaa ya anasa inamfanya kukubali rai ya msichana anayetaka kucheza naye, lakini anamgeuka baadaye. Kumbe ni Bi. Kizee aliyejipodoa. Anajipata mikononi mwake, ambapo anajinasua kwa kulipa salio la mshahara wake kwa ajili ya huduma alizopewa.
ii. Mapenzi na Ndoa.
Ndoa kuu katika hadithi hii ni kati ya Tembo na Emmi. Inakumbwa na misukosuko kadha wa kadha. Wamejaliwa wana ambao hata Tembo hajui wanakula nini. Amewatelekeza kabisa. Mkewe hata anamwomba ampe talaka, yuko tayari kuwalea watoto wao pekee yake. Tembo anaamshwa na mkewe asubuhi ya saa nne ili kupata kiamsha kinywa. Anapomaliza saa sita, anaondoka bila kumuaga, akihofia kuulizwa maswali kuhusu kule anakokwenda. Hana mapenzi ya dhati kwa mkewe wala hamjali.
Tembo anaporudi nyumbani kutoka kwenye mtindi, anavua nguo na kulala. Anagutushwa na ukemi wa mkewe. Amebeba nguo zake zenye alama za midomo. Kabla ya kumsaili, anagundua anahitaji dharura ya matibabu na hapo anamshughulikia mara moja. Tembo anamshukuru kwa hilo.
Dhamira kuu ya barua hii ni Tembo kumwomba msamaha mkewe. Anamwachia shamba lake lenye rutuba. Anahofia huenda amenyakuliwa na maharamia. Anahisi kwamba ndiye tu amebaki, akimwomba arejee kwake ili kumpa tumaini. Anamtaka kuwasalimia nduguze na wanawe, na hata awalete apate kuwaona afarijike. Anatamatisha kwa kusema anampenda.
iii. Ulevi
Tembo amezama katika ulevi na ndio unamletea madhara yote aliyo nayo. Hana uwezo wa kuona. Yuko hospitalini hali hoi. Salim pia yuko hospitali hiyo hiyo, ni mwathiriwa mwenzake.
Anapoamshwa na mkewe, Tembo anakunywa staftahi hadi saa sita kisha kuondoka bila kumuaga mkewe anayechoma mahamri jikoni. Anahofia maswali ya wapi anaenda kwani anajua anaelekea kwenya anasa za ulevi. Anapofika huko anawapata wenzake wanaokunywa kwa kikoa, kila mmoja akichangia zamu yake. Mazingira wanapolewa yanatia kinyaa lakini kwao si hoja.
Pombe inasababisha mauti ya Moshi. Wakiendelea kunywa, anaanguka ghafla na kuanza kurusharusha miguu na kugaragara chini huku povu likimtoka. Hatimaye anafariki hapo hapo. Inagunduliwa kuwa pombe waliyokunywa ilitiwa dawa ya kuhifadhia maiti, tena ilikuwa na maajabu kama panya wa kuoza, nyoka wafu, sodo na nguo za ndani. Tembo anakiri kwamba pombe hiyo, ambayo inapatiwa majina kama chang’aa, tear gas, moshi na mengine ni sumu, ambayo wanatoa pesa zao kuinunua, tena kwa hiari yao. Hana huruma kwa mama pima aliyetupwa korokoroni. Anaiona kuwa stahiki yake.
Licha ya kisanga cha Moshi, bado kiu ya pombe haiwaruhusu kupata hofu. Tembo anaandamana na wenzake kuzima kiu yao kwingine. Huko, wanalewa na kuanza kucheza densi. Anaanguka mtegoni wa Angelica, ambaye anamfyonza salio lake la mshahara kwa huduma za chumbani.
Kutokana na ulevi, hata hagundui kwamba nguo zake zina alama ya midomo, wala hajui zilifikaje huko. Anapomsikia mkewe akipiga ukwenzi, ndio kwanza anagundua, na anajua ana maswali ya kujibu. Hata hivyo, mkewe anagundua anahitaji dharura ya matibabu na kumshughulikia. Haoni, magoti hayana nguvu, mishipa ya damu nayo inazizima. Tembo anasema waliolala bila kuamshwa hawajaamka hadi leo, wengi wamefukiwa.
francis1897 answered the question on January 30, 2023 at 08:56