Get premium membership and access questions with answers, video lessons as well as revision papers.

Je, anwani Pupa inafaa? Fafanua.

      

Je, anwani Pupa inafaa? Fafanua.

  

Answers


Francis
Ina maana ya papara au haraka katika kutekeleza jambo. Ina madhara mengi, mazuri na mabaya. Kuna methali isemayo kwamba mwenye pupa hadiriki kula tamu.
Mwakuona anapokutana na Bi. Mtego na kusikia nia yake ya kumpeleka ng’ambo kufanya kazi, anamezwa na pupa na kukubali masharti yake mengi bila kuyawazia sana. Anaiona hii kama fursa yake ya kuwa na maisha mazuri na kusaidia familia yake pia. Bi. Mtego anampa simu ambayo anafaa kuificha na kuitoa faraghani. Haifai kuonekana na yeyote, hata msiri wake wa karibu zaidi wala wazazi wake. Anaificha kusikoweza kufikika na mikono ya ziada.
Anaposubiri kwa wiki, muda huu anauona kama mwaka kutokana na pupa aliyo nayo kwenda ng’ambo. Anahiari kuacha hata familia yake na masomo yake.
Mwakuona anaondoka nyumbani kwa pupa siku ya miadi kwa jitihada tele kufika mjini, anakofaa kukutana na Bi. Mtego. Anajifichaficha na kuwahadaa watu hadi hatimaye anapofika mjini. Anabadili sare na kuvaa mavazi aliyopatiwa na viatu, kisha kumpigia simu wakala wake. Anashangaa kwa nini mhisani wake ndiye anamtumikia. Hata hivyo, pupa haimruhusu kuchunguza hilo. Anaona ng’ambo tu!
Katika matayarisho, anafanyiwa mengi. Anatengenezwa nywele na kukandwa kisha kulainishwa ngozi. Anahudumiwa kwa muda wa majuma sita pamoja na wenzake, huku wakilishwa vyakula vizuri. Huduma zote hizi ni za bure. Wanarembeshwa zaidi na kuvikwa mapambo ya kila nui. Haya yote hayamtumi kushuku unachoandaliwa, akili yake inalenga ng’ambo bado.
Muda wote wa matayarisho, hajamwona wala kuwasiliana na Bi. Mtego. Simu nayo ilikuwa keshachukuliwa. Hayo hayamtumi kuwa na maswali yoyote. Hata anapogundua kwamba amevishwa nguo fupi, anawaza labda ndio ustaarabu wa ng’ambo. Hata anabebwa na dereva wake peke yake. Anatarajia kuona uwanja wa ndege baada ya kutoka hapa.
Mwakuona anapofika Chenga-ways, anauliza kuhusu safari yake ya ng’ambo. Vicheko vya wanawake nyuma ya kaunta havimgutushi kuhusu shughuli za huku. Hata anapoitwa, anainuka kwa furaha na kiherehere kumfuata mwelekezi. Anatarajia kupelekwa kwenye uwanja wa ndege na kusahau shughuli za pale. Akilini, imejaa taswira ya ng’ambo.
Mwakuona anapambanukiwa na mambo anapojikuta ndani ya chumba mikononi mwa mwanaume, tena mlango ushakomelewa. Hana la kujinasua, bali inamlazimu kukubali matokeo. Sasa anagundua jinsi pupa ilivyomziba macho na kumweka hatarini. Pupa ya kutoroka inampata Mwakuona, na inatiliwa mkazo na rafiki yake Mashaka, anayemweleza hali iliyomkumba.
Wanakubaliana kuhepa kwa vyovyote vile na kusaka haki kwa ajili yao na pia kwa ajili ya wenzao. Anamlaumu Bi. Mtego, mwenye Chenga-ways na wateja wa pale, na pia serikali kwa kufumbia macho biashara kama hizi. Lakini anaapa jambo moja, chuma chao ki motoni!
Anakumbuka ushauri wa mwalimu wake Bw. Mpevu kuhusu kufanya maamuzi yanayofaa katika maisha yao. Anashangaa kwa nini hakufuata ushauri wake, msichana wa kidato cha tatu pale alipo, akadanganyika kwa urahisi hivyo. Anakiri kwamba ni pupa imemwingiza humu na kujilaumu, lakini anaamua kupambana kujitoa. Anashangaa iwapo wasichana walioandaliwa pamoja hakuna aliyejua yanayowasubiri. Haikosi nao pupa iliwaziba macho.
Pupa inamwezesha kutoroka Chenga-ways. Anaingia msalani usiku wa manane na kutoka kwa haraka kupitia kwenye tundu lililoachwa na bati lililobambatuka. Licha ya kufaulu, anakwaruza na kuvuja damu. Anatoka na kutafuta viatu alivyotangulia kutupa nje na kupata kimoja. Anakichukua na kutoka mbio. Anapitia upembe wenye giza asionekane.
Japo wamemwandama, bado ana pupa ya kutekeleza maaganao yake na Mashaka. Anaazimia kufika nyumbani na kuomba msamaha, japo hajui iwapo watampokea. Anaazimia pia kutafuta kituo cha polisi kutafuta haki, na pia kituo cha habari kuwaanika wale mahasidi. Kunapopambazuka, anakuona mwinamo kwa mbali. Kuna tumaini.
Pupa pia ndiyo inamsukuma Bi. Mtego kumtendea Mwakuona unyama ule. Anamhadaa kwa ahadi za ng’ambo. Nia yake ni kunufaika kwa malipo kutokana na biashara hii haramu. Ana pupa ya kupata hela za haraka. Wateja wa Chenga-ways pia wana pupa ya mahaba. Wanachagua wasichana kati ya wanaocheza densi mbele yao na hata kuwalipia kwa ajili ya huduma zao. Pupa inawatuma kuwaharibia maisha wasichana kwa kuwakatizia masomo na kuwadhulumu kimapenzi.
francis1897 answered the question on January 30, 2023 at 11:38


Next: Huku ukitolea mifano, eleza matumizi ya mbinu zifuatazo katika hadithi, Nilitamani; (i) Kinaya (ii) Taharuki (iii) Taswira
Previous: Umaskini na usherati ni baadhi ya mambo ambayo hudidimisha maendeleo. Thibitisha kauli hii ilivyotumika katika hadithi, Pupa.

View More Kiswahili Fasihi Questions and Answers | Return to Questions Index


Learn High School English on YouTube

Related Questions