Taja baadhi ya masuala muhimu katika uchambuzi wa mashairi

      

Taja baadhi ya masuala muhimu katika uchambuzi wa mashairi

  

Answers


Francis
Anwani/kichwa cha shairi
Maswali mengi huwahitaji wanafunzi kulipa shairi anwani mwafaka. Je, ni vipi mwanafunzi ataweza kulijibu swali hili? Uteuzi wa anwani huzingatia urudiaji wa maneno fulani katika shairi lote au pia kibwagizo. Hivyo basi mwanafunzi anaweza kulipa shairi anwani kwa kuzingatia ni maneno yapi yaliyorudiwarudiwa au kwa kutumia maneno katika kibwagizo.
Anwani pia yaweza kubuniwa kutokana na maudhui yanayojitokeza kwa wingi katika shairi. Anwani ya shairi huwa kama ufupisho au muhtasari wa yale yaliyomo katika shairi. Hivyo basi mtu yeyote anayesoma kichwa cha shairi fulani huweza kukisia kile ambacho shairi hilo linazungumzia hata bila ya kulisoma shairi lenyewe. Kwa ufupi, kichwa cha shairi humpa msomaji taswira ya kijumla ya mambo yanayozungumziwa katika utungo wenyewe.

Falsafa ya mwandishi
Huu ni msimamo wa mwandishi kuhusu maudhui tofauti tofauti aliyoyajadili katika utungo wake. Msimamo wa mwandishi unaweza kuwa analiunga mkono jambo fulani au analipinga jambo fulani. Hili litadhihirika wazi jinsi anavyoeleza maudhui yake.

Nafsineni
Huwa ni anayezungumza katika shairi. Wakati mwingine huwa ni mtunzi mwenyewe anayezungumza au wakati mwingine akamtumia mhusika fulani kupasha ujumbe wake.

Nafsi nenewa/hadhira lengwa
Huwa ni anayeelekezewa ujumbe. Ujumbe katika shairi au hata kazi yoyote ya fasihi huwa inamlenga mtu au kundi fulani la watu. Walengwa hawa ndio nafsi nenewa ama hadhira lengwa, kwa mfano wanafunzi, wazazi au wananchi.

Lahani/Toni ya shairi
Mwanzoni mwa kitabu hiki tulieleza kuwa shairi hutumia lugha teule, yenye mnato na iliyojaa hisia. Toni ni hisia ambazo huibuka kutokana na yale anayosema mzungumzaji katika shairi. Mzungumzaji huweza kuibua hisia za kuchekesha, kulalamika, kubeza, furaha, huzuni n.k

Mandhari na wakati
Mandhari ni mazingira au muktadha au mahali ambapo shairi fulani hutungiwa. Mandhari na wakati huenda sambamba. Kutokana na maudhui ya shairi, tunaweza kubaini ni wapi na ni lini shairi lilitungwa. Mifano ya mandhari ni kama vile Pwani, mjini, shuleni n.k. Hivyo basi mandhari na wakati husaidia kuendeleza maudhui ya shairi. Kwa mfano katika shairi la Mnazi na Vuta n’ kuvute, mandhari ni ya Pwani.

Uhusika katika ushairi
Mashairi pia huweza kuwa na wahusika haswa tukirejelea ngonjera na malumbano hivyo basi ni muhimu kulitilia maanani suala hili. Wahusika huwa kama sauti ya mwandishi maanake ni kupitia kwao ambapo mtunzi hueleza mawazo yake bayana.

Tasnifu
Haya ni maelezo mafupi ambayo mwandishi wa kazi ya fasihi huyatoa kuhusu maudhui na dhamira yake katika utungo.

Lugha ya nathari/Lugha tutumbi/mjalizo
Hili ni swali ambalo aghalabu halikosi kwenye maswali ya ushairi. Mwanafunzi ataulizwa...Andika ubeti fulani katika lugha ya nathari. Lugha ya nathari ni lugha ya kawaida. Huwa ni maandishi mfululizo. Ubeti uandikwe kwa aya moja ama kwa njia ya kiinsha bali si ya kishairi. Mishororo igeuzwe iwe sentensi za Kiswahili sanifu zinazozingatia kanuni za lugha. Sehemu zilizorudiwarudiwa ziandikwe mara moja tu. Usitumie lugha ya mshairi.
francis1897 answered the question on February 1, 2023 at 08:24


Next: Taja aina mbalimbali za takriri katika ushairi
Previous: Eleza mambo yanayozingatiwa katika uhuru wa kishairi

View More Ushairi Questions and Answers | Return to Questions Index


Exams With Marking Schemes

Related Questions